MAADILI( CULTURE)

Mwingilisti
Clint Rogers akihubiri wakati kulia kwake ni mwenyeji wake Mch Jared Mlongecha akitafsiri mahubiri yake kwa lugha ya Kiswahili
NA KENNEDY SIYAME,
FEB 8, 2008.
Boston, MA, USA
Waafrica wanaoishi nchini Marekani wametakiwa kuyalinda na kuyaenzi maadili ya tamaduni za nchi zao wakati wao wote watakaofanikiwa kuishi nchini humo badala ya kukimbilia kuiga na kutamani kudumisha tamaduni za kigeni ambazo nyingine zina dhalirisha utu wao.
Rai hiyo imetolewa na mwinjilisti Clint Rogers wakati wa mahubiri yake Jan20,08 kwenye kanisa la kimataifa la kiinjili(International Gospel Church) lililopo kwenye eneo la Chelsea katika mji wa Boston, Massachusetts, nchini Marekani baada ya kuarikwa na mwenyeji wake Mch.Jared Mlongecha.
Katika mahubiri yake mwinjilisti Rogers ambaye aliongozana na mke wake Angela alisema inapendeza kuona kuwa mtu anabakia katika maadili ya nchi yake mahali popote anapoamua kuishi na kwamba hiyo ndio njia pekee inayoweza kutambulisha utamaduni wake na pia anakuwa anauheshimu uumbaji wa Mungu.
“Nataka niwaambie ninyi ndugu zangu kwamba kuleni hamburger, na vyakula vingine vyote mtakavyovipenda hapa Marekani, lakini nawasihi mmbaki vivyohivyo na uafrika wenu wala msitamani kuwa wamerekani”alisema mwinjilisti Rogers na kuongeza “mtu anapendeza anapobaki katika asili yake na wala sio kuanza kutamani kuiga asili na tamaduni za mtu mwingine”.
“Mimi ni mmarekani na nitabaki mmarekani siku zote na sikotayari kuiga uafrika na siwezi kuwa mwafrika hata siku moja”aliendelea kusisitiza Mwijilisti Rogers na kusema “kama ni kuimba na kucheza imbeni na kucheza kama waafrika na wala sio vingine vyo”alisema Bw.Rogers.
Baadhi ya waafrika waliojaliwa kuingia na kuishi nchini Marekani wamekuwa wakiukaji wakubwa wa maadili, mila na desturi za nchi zao kwa kutaka kuiga na hata wengine kujaribu kujifanya wamarekani kwa tabia,wakitamani kuishi kama wao.
Baadhi ya mambo ambayo baadhi ya waafrika wanaoishi nchini hapa wamekuwa wakiyaiga ni pamoja na kuwapa taraka waume zao na kisha kuwadai pesa za kujikimu na za malezi ya watoto ambazo huwasaidia kununulia magari ya kifahali na kuishi maisha ya anasa.
Mambo mengine ambayo wamekuwa wakiyaiga baadhi ya waafri ka waishio nchini hapa ni pamoja na uvutaji wa sigara wakupindukia kwa akina baba, mama na watoto, kuvaa nguo nusu uchi hata mbele ya watoto, kupeana busu za kimapenzi hadharani tabia ambazo kwa mwafrika ni aibu na wala hazikubaliki katika jamii.
Kuhusu mahubiri yake ya siku hiyo,Mwinjilisti Rogers aliwataka waumini kuwa na imani katika Mungu waliomwamini hali wakijua kwamba yeye ni mwaminifu na yuko makini kutimiza ahadi zake.

Kushoto ni Ebochwa Mlongecha akipioga ngoma za umeme akisaidiwa na Gabriel Kisaboo (aliyesimama pichani) katika midundo ya kiafrika wakati wa mkutano wa ndani wa mwingilisti Clint Rogers muda mfupi kabla ya kuanza mahubiri |

Kikundi cha waimbaji wa kanisa la International Gospel (IGC) wakiwa kwenye uimbaji wa pamoja na mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili Shikoh kutoka Kenya muda mfupi kabla ya mahubiri ya Mwinjilisti Clint Rogers |
“Unajua huyu Mungu mliyechagua kumwamini, nilazima atofautiane na Miungu mingine na ndipo hapo anapojulikana kuwa ni Mungu aliye hai na anayetofautiana na wengine”, alisema Rogers.
Akitumia maneno ya Mungu kutoka katika kitabu kitakatifu cha Biblia, Alisema imani ya wale watu waliombeba mgonjwa wao na kumfikisha kwa Bw.Yesu kupitia darini ilisababisha uponyaji kwa mtu wao na kwamba hata Yesu pamoja na mkutano wake waliiheshimu nia na imani yao.
Alisema siku hizi waumini waliowengi wanaingia makanisani bila kujua wanachokwenda kufanya zaidi ya kufurahia uimbaji na kucheza kutokana na uzuri wa midundo ya miziki inayopigwa na kwamba baada ya hapo wanakuwa hawana la kufanya.
“Wapo wagonjwa wengi leo makanisani ambao wameokoka na wanasema Yesu anaponya lakini wao bado ni wagonjwa, nasema kama Yesu yuko hai ni lazima aponye wagonjwa, afufuewafu, ainue viwete na kufumbua macho ya vipofu”alisema Bw.Rogers na kuongeza kuwa hizo ndio kazi zake zinazomtofautisha na miungu wengine.

Pichani ni baadthi ya waumini na wageni kutoka maeneo mbalimbali wakimsikiliza mwinjilisti Clint Rogers wakati wa mahubiri yake yeye mwenyewe hayupo katika picha hii. |

Mke wa mwinjilisti Angela Rogers akifuta machozi ya furaha muda mfupi baada ya kupokea zawadi ya mkufukutoka kwa mmoja wa waumini wa kanisa la IGC |
Akihitimisha mahubiri yake katika kanisa hilo, Mwinjilisti Rogers alifanya maombezi maalum kwa magonjwa sugu ambapo Mch.Douglas Whitlow ambaye amekuwa akisumbuliwa na figo kwa muda mrefu alipokea uponyaji wake pamoja na Purity Munyu ambaye aliponywa sikio wakati Jaqueline Owuri aliponywa mguu.
Mtu mwingine aliyepokea uponyaji siku hiyo ni kijana Shaqwille Pinckney ambaye alikuwa na tatizo la uyeyushaji wa chakula katika utumbo wake baada ya kununua na kula vyakula ambavyo hapo awali alikuwa hawezi kula.
Wakati huohuo Mwinjilisti Clint Rogers amethibitisha kwamba anampango wa kuanza ziara ya mikutano ya injili katika sehemu mbalimbali za bara la Afrika hususani katika nchi za Afrika mashariki na kati ambapo July mwaka huu atakuwa na mikutano katika nchi za Tanzania, Kigoma na Burundi.
Bw.Rogers amethibitisha nia yake ya kutembelea bara la Afrika kwa ajili ya injili wakati akihubiri katika ibada maalumu ya mkutano wake kwenye kanisa la kiinjili lililopo nchini Marekani Jan20, 2008 na kwamba ameamua kufanya hivyo kutokana na mapenzi yake ya dhati aliyonayo kwa bara la Afrika.
Kanisa la kimataifa la kiinjili lililopo Chersea nchini Marekani, linawakusanya waafrika wengi wanaoabudu mahali hapo kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Congo DRC na Burundi,Waafrika wengine ni kutoka nchi za Kameruni na Heiti.
MWISHO.
NA KENNEDY SIYAME, USA.FEB 6,2008.
|